Waziri wa ulinzi wa Marekani Ash Carter ameitisha mkutano usio wa kawaida nchini Kuwait wa wataalamu kijeshi, kidiplomasia na kijasusi Wamarekani kuhusu mkakati wa serikali wa kukabiliana na machafuko na kuenea kwa ushawishi wa kundi la kigaidi la Daesh. Carter amewaita majenerali kadhaa wa ngazi ya juu wa jeshi la Marekani, wajumbe wa rais Barack Obama, John Allen na Brett McGurk, pamoja na mabalozi wa Marekani nchini Jordan, Saudi Arabia na mataifa mengine ya kiarabu. Mkutano huo wa faragha unaanza leo katika kambi ya jeshi ya Arifjan, ambako Luteni Jenerali James Terry wa jeshi la Marekani anaongoza kampeni ya kijeshi dhidi ya kundi la kigaidi la Daesh linalojiita Dola la Kiislamu. Jumla ya wajumbe 30 wanatarjiwa kuhudhuria mkutano huo unaofanyika huku kukiwa na ukosoaji mkubwa kutoka kwa chama cha Republican wa mkakati wa rais Obama wa kupambana na itikadi kali za dini ya kiislamu.
Na huko Yemen rais wa Yemen Abedrabbo Mansour Hadi ameongoza mkutano wa magavana katika mji wa Aden, kusini mwa Yemen huku akianza kutekeleza majukumu yake baada ya kutoroka kutoka kifungo cha nyumbani katika mji mkuu Sanaa. Kiongozi huyo anayeungwa mkono na nchi za Magharibi alikimbilia Aden Jumamosi iliyopita baada ya kutoka kisiri katika makazi yake mjini Sanaa ambako alikuwa akizuiliwa na kundi la wanamgambo wa kishia wa Huthi ambalo linaudhibiti mji huo. Gavana wa jimbo la Aden Abdulaziz bin Habtoor amesema baada ya mkutano huo wa jana kwamba rais Hadi ataendeleza juhudi za kuiongoza Yemen kutoka Aden. Mkutano huo ulihudhuriwa pia na wakuu wa jeshi na idara za usalama.
Kundi la Mashia la Houth limeshika hatamu za uongozi wa Yemen baada ya serikali ya rais Hadi kupanga kuigawa Yemen kwa misingi ya kikabila na madhehebu, jambo ambalo lingepelekea hatari kubwa katika nchi hiyo.